Tuesday, December 08, 2009

 

Mangula auchambua
uongozi wa Kikwete

Sadick Mtulya
UTAWALA wa Rais Jakaya Kikwete umezidi kukosolewa baada ya katibu mkuu wa zamani wa CCM, Philip Mangula kuuchambua, akisema unasumbuliwa na mambo matatu makubwa, ikiwa ni pamoja na kupeana uongozi kwa urafiki.
Mangula anaendeleza mjadala wa siku za karibuni ambao umekuwa shubiri kwa CCM, ambayo imelazimika kutoa kauli kadhaa kujibu mashambulizi dhidi ya mwenyekiti wake.
Makada wa mwisho kuikosoa serikali ya Kikwete walikuwa mawaziri wa zamani, Matheo Qares na Juma Nkangaa ambao walieleza wasiwasi wao kama mkuu huyo wa nchi ana uwezo wa kufanya maamuzi magumu na kwamba CCM imepoteza mwelekeo kwa kuamua kukumbatia wafanyabiashara na kuachana na sera yake ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi.

Safari hii, Mangula ambaye alikuwa mtendaji Mkuu wa CCM kabla ya kuteuliwa kwa Makamba, ameibuka na kueleza udhaifu wa chama hicho tawala na kikongwe barani Afrika na ambacho hakuna shaka kwamba kinapitia kwenye wakati mgumu kwa sasa.

Mangula ambaye alihudhuria kongamano la Mwalimu Nyerere jijini Dares Salaam ambalo liliibua hoja nyingi dhidi yab serikali ya Kikwete wiki iliyopita, hakuchangia maonin yake katikam mjadala huo, lakini
baadaye alifanya mahojiano na Mwananchi na kutaka mambo matatu ambayo yanautafuna uongozi wa Rais Kikwete.

Mangula alitaja mambo hayo kuwa ni ubinafsi, kufanya maamuzi kabla ya kuelimisha wananchi na kuwepo kwa wigo finyu wa majadiliano na wadau katika masuala mbalimbali.

Mangula, ambaye alishika nafasi ya katibu mkuu wa CCM kwa kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa serikali ya awamu ya tatu, alitahadharisha kuwa iwapo mambo hayo hayatarekebishwa kwa haraka na kwa kipaumbele kinachostahili, taifa litaelekea pabaya zaidi.

“Utawala wa sasa umetofautiana na tawala nyingine kwa kupungukiwa na mambo matatu ya msingi ambayo ni ubinafsi, kufanyika maamuzi kabla ya kuelimisha wananchi pamoja na kutokuwepo kwa wigo mpana wa majadiliano kuhusu masuala mbalimbali ya mustakabali wa taifa,” alisema| Mangula.

Mangula alisema hali hiyo imesababishwa na watu wengi wanaopewa uongozi kutokuwa sifa za kuongoza na kwamba wamepata nafasi hizo kwa njia za urafiki.

“Hata utaratibu mzima wa kuwapata viongozi wanaostahili kwa sifa haupo, badala yake mambo yanafanywa kwa urafiki,” alisema Mangula ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu.

Akifafanua hoja zake hizo, Mangula alisema katika utawala wa sasa ubinafsi ndio umeonekana kuchukua kipaumbele katika kutatua mambo muhimu ya kitaifa.

Mangula aliweka bayana kwamba katika utawala uliopita ubinafsi haukupewa nafasi kwa kuwa kabla kiongozi hajazungumzia jambo lolote, alilazimika kupata mawazo ya chama tawala na wanachama kuhusu anachotaka kuzungumza.

Aliongeza kwamba kutotumika kwa mfumo huo ndio sababu ya kupishana kwa kauli za viongozi kunakoendelea kutamba kwenye safu za mbele za vyombo vya habari kwa sasa.

“Tabia ya kutaka kuonekana kuwa wewe ni bora kuliko mwingine ipo, ndio maana leo viongozi, tena wa kutoka chama kimoja, wanapishana kauli kuhusu jambo moja,” alifafanua.

Akizungumzia kufanyika kwa maamuzi kabla ya kuwaelimisha wananchi, Mangula alisema hilo ni tatizo linaloendelea kulalamikiwa na Watanzania.

Mangula alisema katika utawala uliopita watu walielimishwa kwanza kabla ya kufikiwa kwa maamuzi.
“Utaratibu wa kuelimisha kwanza kabla ya kufikiwa kwa maamuzi ndio uliokuwa ukitumika, lakini hali sasa inaonekana kuwa tofauti,” aliongeza.

Kuhusu kutokuwepo kwa wigo mpana wa majadiliano katika masuala ya kitaifa, Mangula alisema hiyo inatokana na viongozi wachache waliopewa dhamana na wananchi kuamini kuwa mawazo yao yanajitosheleza.

Hoja za Mangula, ambaye kwa sasa anajishughulisha na masuala ya kilimo, zinashabihiana na zile zilizowahi kutolewa na mawaziri wakuu wawili wastaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba kuhusu mustakabali wa taifa.

Jaji Warioba alinukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni akitahadharisha kuwa nchi inaelekea kubaya kutokana na mambo mbalimbali kuendeshwa kinyume.

Warioba, ambaye alishika nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa serikali kwenye miaka ya themanini, alifafanua kuwa taifa linakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo ukosefu wa maadili ya uongozi, rushwa na hata utaratibu mzima wa kuendesha mambo na kubainisha kuwa kuna pengo kubwa katika kuaminika kwa serikali.

Naye Dk Salim Hamed Salim, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Afrika (OAU), alisema mfumo wa serikali ya Tanzania kwa sasa umeoza kwa rushwa na hivyo hauwezi kumsaidia rais kuikabili, hivyo rushwa kutawala kuliko kitu kingine.

Dk Salim alisema wakati wa utawala wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere, rushwa ilidhibitiwa kikamilifu, lakini wakati huu rushwa imeachiwa nafasi kubwa na kufanya hali ya Watanzania idorore.

Alisema tofauti kubwa kati ya awamu hizo na ile ya Mwalimu Nyerere ni kuwa muasisi huyo wa taifa alionyesha kwa vitendo kuwa rushwa ni jambo aliloamua kulifungia mkanda na kupambana nalo, lakini baada ya hapo tatizo hilo limeachiwa liendelee kiasi cha rushwa kugeuka kuwa utaratibu.

Mwanadiplomasia huyo aliongeza kwamba, licha ya nia njema ya Rais Kikwete ya kupambana na rushwa na ufisadi, bado mfumo mzima wa serikali umeoza kiasi ambacho haiwezekani kupambana na rushwa.

Baadaye wakati wa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Qares, ambaye alikuwa Waziri wa Menejimenti ya UItumishi wa Umma katika serikali ya awamu ya tatu, na Nkangaa ambaye alikuwa waziri katika serikali ya awamub ya pili, waliibuka.

Qares alimtaka Rais Kikwete awe jasiri na kufanya maamuzi magumu na akashauri kuwa akishindwa kufanya hivyo hadi 2010, CCM isimpitishe kugombea urais 2010.

Qares, ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wakati wa uongozi wa Benjamin Mkapa, alisema Rais anapaswa kufumba macho na kuwashughulikia hata wale wanaosema hakukutana nao barabarani.

Naye Nkangaa alisema CCM imepoteza heshima yake na kubaki kuwa chama cha matajiri wachache na kutupa mkono wakulima na wafanyakazi, ndiyo maana inasuasua kuwachukulia hatua watuhumiwa katika kashfa za Kagoda na Richmond.

Tangu kutolewa kwa ripoti ya kashfa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond, wabunge wa CCM wamekuwa wakitofautiana sana katika hoja, baadhi wakiunga mkono kujiuzulu kwa Edward Lowassa katika nafasi ya uwaziri mkuu na kutaka hatuia zaidi zichukuliwe, huku wengine wakipinga.
Hali ilizidi kuwa mbaya katika mkutano uliopita wakati wabunge walipoicharukia serikali yao wakiituhumu kufanya mambo kwa ubinafsi na kubariki mikataba mibovu, na mjadala huo uliilazimisha CCM kuitisha mkutano wake wa Halmashauri Kuu.
Lakini mkutano huo ukawa moto mbaya zaidi baada ya Spika Samuel Sitta kunusurika kuvuliwa uanachama kutokana na kundi linalotuhumiwa kwa ufisadi kujipanga vyema kushughulikia wanaowatuhumu.
Mijadala mikali kwenye kikao cha Halmashauri Kuu iliisha kwa CCM kuunda kamati ya wazee wa busara, ikilongozwa na rais wa serikalinyab awamu ya tatu, Ali Hassan Mwinyi ambayo mwezi uliopita ilisababisha kizaazaa kingine wakati ilipoongea na wabunge kuhusu kudhoofika kwa mahusiano baina ya wanachama na viongozi wa chama hicho tawala.
Lakini mkutano huo ukawa jukwaa zuri kwa watuhumiwa wa ufisadi kujibu mashambulizi yanayotolewa kila mara hadharani dhidi yao na hasa kwenye vikao vya Bunge.
Katika mikutano hiyo ya Kamati ya Mwinyi, makamanda wa vita dhidi ya ufisadi walijikuta wakibebeshwa tuhuma nzito na kutolewa maneno machafu, kiasi kwamba hali ndani ya CCM ikaonekana kuwa si shwari na haikuwa ajabu wakati mawaziri hao wa zamani pamoja na Mangula kujitokeza na kuuchambua utawala wa Kikwete kuwa una matatizo.

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?