Monday, July 23, 2007

 

Kuna nini Yanga na Micho?

Moja ya mambo yanayokera kwa sasa ni kutokuwepo kwa habari z auhakika kuhusu mustakabali wa kocha Mserbia, Sredojevic Milutin Micho, ambaye taarifa rasmi zinasema tu amekwenda kwao kwa mapumziko baada ya kumalizika kwa Ligi Ndogo.
Pia kocha huyo amesema amekwenda kwao kwa matibabu baada ya hali yake kutetereka kutokana na kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu wakati timu ikiwa kambini mjini Arusha.
Kwa kawaida kurejea kwa kocha kama huyo hakuwezi kuwa siri ya ajabu kiasi cha kuwafanya viongozi wasite kutoa kauli thabiti kuwa atarudi tarehe fulani. Kutokuwepo kwa taarifa za kueleweka kunasababisha kuzuka kwa ubashiri tofauti kuwa huenda akawa ametimka kama ilivyokuwa kwa kocha Neider Santos kutoka Brazil, ambaye ligi ilipoisha alisema anarejea kwao kwa mapumziko, lakini baadaye akasema ameshatimka.
Wengi wanaona kama kutofanya vizuri kwa Micho katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, baadaye Kombe la Shirikisho na kupoteza ubingwa wa Bara kwa kufungwa na Simba katika fainali ndivyo vitu vinavyoweza kuwa vimemtimua Mserbia huyo, aliyewahi kuzifundisha Orlando Pirates, Sports Club Villa na St George ya Ethiopia.
Lakini wengine pia wanahisi kuwa huenda mkataba wake wa siri, ambao ulielezwa kuwa wa miaka mwili, pengine ulimpa majukumu ya kuhakikisha Yanga inafika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa na kutetea ubingwa wa Bara, na kama si hivyo, basi utakuwa umekatizwa.
Hakuna anayejua kwa undani mkataba huo unazungumzia nini, hasa kutokana na usiri wa mikataba ya Kitanzania.
Lakini pengine ni muhimu kwa uongozi wa Yanga kujitokeza na kuzungumza kwa uhakika kuwa kocha huyo amekwamishwa na kitu gani na atarejea lini hasa badala ya kuachia taarifa za kurejea kwa kocha huyo kuzagaa ovyo na kuzusha ubashiri ambao unaweza hata kuvuruga maandalizi ya klabu hiyo kwa michuano ya Kombe la Tusker.
Hata uongozi ukisema Micho ndio ameondoka kabisa, nani atawalaumu kwa kuwa huo ndio utakuw auamuzi wake. Na kama atarejea lini, pia watu watakubali. Hakuna haja ya kulifanya suala la Micho kuwa kubwa wakati uongozi unajua kinachoendelea.

Sunday, July 22, 2007

 

Ujambazi

Wanasema majambazi hawapendi wasimangwe wala waonywe. Kila inapotokea wanaonywa kuwa wajisalimishe, basi ndio huibuka kwa nguvu mpya na vitimbi vya aina yake. Baada ya mheshimiwa Jakaya Kikwete kutoa onyo akiwa kule Mwanza, matukio ya ujambazi yameripotiwa mengi kuliko kiasi, yakihitimishwa na tukio la aina yake la kule Arusha ambako inaonekana kama ilikuwa ni sinema ya action.
Sisi wa Tabata usiku wa jana tulionjeshwa milio kama minne ya bunduki wakati majambazi walipovamia pale kwenye kituo cha mafuta cha Kimanga. Huko wamejeruhi na kuvunja kontaina na kuondoka na walichokikuta, wakati asubuhi hii tumesikia kuwa wamefanyiza huko Chanika.
Bahati nzuri leo hii waziri anayehusika na usalama wa raia ndio anawasilisha hotuba yake ya bajeti. Sijui atakuwa ametuandalia nini kinachohusiana na matukio ambayo yametokea baada ya hotuba yake kuandikwa. Maana wakati akiiandaa, matukio hayo yalikuwa yametulia kiasi cha kuonekana kana kwamba polisi imedhibiti matukio ya ujambazi.
Sijui atatumia njia gani kutuliza haya matukio; maana kama akitangaza vita kali dhidi ya ujambazi, basi, kama wale wanaoamini kuwa majambazi hayaki kuonywa, vitendo hivyo vitaongezeka mara dufu. Sijui sisi wa uswahilini itakuwaje. Na kama akitaka kufumbia macho kwa kuogopa majambazi kuchukia, ndio kabisa hali itakuwa mbaya.
Tufanyeje sasa kupambana na hawa watu, tena wale wakali zaidi ni wanaotoka nchi jirani.
Waziri kazi kwako leo. Tunategemea uache kidogo hotuba yako iliyoandaliwa zamani kidogo, na kuzungumza kwa kauli thabiti kuhusu hili wakati utakapokuwa unamalizia kusoma hiyo hotuba, kama vile Mama Sitta alivyofanya kwa kuzungumzia michezo ya umiseta kidogo, katika kile kilichoonekana kuwa ni kutupoza wadau.


Angetile Osiah

 

Salaam

Kwa muda mrefu, nilikuwa nimenyamaza kidogo kutokana na asili ya shughuli zetu hasa wenye wadhifa wa uhariri. Nadhani mnajua namaanisha nini.
Lakini nimerudi kwa nguvu mpya nikiwa na mengi ya kuwapa kuhusu kile kinachoendelea kwenye anga zote, kuanzia masuala ya kimichezo, mitindo, staili, siasa na mambo mengine ya kibongobongo.
Najua pia mtakuwa na mengi ya kunipa hivyo nategemea kuwa tutapashana yale yanayofaa.
Angetile Osiah

This page is powered by Blogger. Isn't yours?