Tuesday, December 08, 2009

 

JK akijibu tu, mipasho itakuwa ruksa





Pichani Rais Kikwete akifafanua jambo wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili jijini Dar es salaam akitokea ziara ndefu iliyohusisha bara la Amerika Kaskazini na visiwa vya Carribea. Kushoto na makamu wa rais, Dk Shein


Rais Jakaya Kikwete jana alirejea nchini akitokea kwenye ziara ndefu iliyomchukua kwenye nchi kadhaa duniani. Alianzia Jamaica akashuka Trinidad na Tobago kabla ya kwenda Cuba ambako alielezea jinsi alivyomuhusudu Che Guevera na baadaye kusogea Marekani kwa uchunguzi wa afya.
Lakini shangwe za mapokezi ziliambatana na maswali juu ya yale aliyoyaacha yakijiri hapa nchini, na hasa ule mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambao ulibua maswali mengi juu ya utendaji wa mkuu huyu wa nchi.
Si kawaida kwa watu, hasa wanaotoka kwenye chama kimoja kuhoji utendaji wa kiongozi wao, lakini mawaziri wa zamani, Matheo Qares, Mussa Nkangaa na katibu mkuu wa CCM wa zamani, Phillip Mangula walieleza hofu yao juu ya utendaji wa rais na mwenyekiti wao wa chama. Na Qares alidiriki kusema kama mheshimiwa hataweza kuchukua maamuzi magumu kabla ya 2010, basi CCM haina budi kutafuta mgombea mwingine wa kiti hicho.
Nkangaa, ambaye pia aliwahi kuwa mbunge mkoani Singida, alieleza kuwa chama kimepoteza hadhi yake na sasa kimesahau wafanyakazi na wakulima na kukumbatia matajiri. Mangula alishangazwa na jinsi chama kinavyoendeshwa kwa sasa.
JK alikumbana na maswali kuhusu masuala hayo yote na kwanza akadokeza kuwa hashangazwi na hao waliosema hayo, lakini pili akatoa neno ambalo limenitia shaka kidogo kwamba atakaa na wenzake - bila ya shaka akina Nkangaa, Qares, Mangula, Salim na Warioba si wenzakew- na kujiandaa kujibu hayo makombora.
Ndipo hapo napojiuliza kama kuna umuhimu kwa JK kujibu maoni ya hao waliokosoa utendaji au kufanya kazi nzuri ili iwe majibu tosha kwa wote wenye mashaka naye.
Nadhani JK akithubutu na kuanza kujibu hayo, atakuwa amefungua jukwaa kubwa la mipasho ambalo halitakuwa na msimamizi maana hata rais na mwenyekiti wa chama tawala atakuwa amejitumbukiza katika kushambuliana.
Ndio maana nasubiri kwamba akijibu tu, basi mipasho itakuwa ruksa

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?