Tuesday, December 08, 2009

 

Ahly, Zamalek ni kufa na kupona leo





Na Mwandishi Wetu
MACHO ya mashabiki wa soka ambao daima huvutiwa zaidi na upinzani wa klabu zinazotoka mji mmoja, leo yataelekezwa Cairo nchini Misri ambako Al Ahly itakuwa ikipambana na Zamalek katika mechi ya daby ambayo inachukuliwa kuwa ina vurugu kubwa kuliko nyingine zote duniani.
Mechi hiyo baina ya timu za jijini Cairo itakuwa ya pili baina ya vigogo hao msimu huu baada ya kushindwa kufungana katika mechi ya kwanza iliyochezeshwa na mwamuzi kutoka Ubelgiji, Frank de Bleeckere.

Mbelgiji huyo atapuliza filimbi tena leo wakati Al Ahly, klabu yenye mafanikio kuliko zote barani Afrika, itakapovaana na wapinzani wao wakubwa wa jijini Cairo.

Kwa sasa Ahly inaongoza msimamo wa ligi kwa tofautin ya pointi tano, ikifuatiwa na Ismailia na ndiyo inayopewa nafasi zaidi ya kuibuka kidedea dhidi ya Zamalek, ambayo imepoteza mechi tatu zilizopita na ambayo iko juu kidogo ya timu zilizo hatarini kushuka.
Kocha mpya wa Zamalek, Hossam Hassan ana wasiwasi na wachezaji wake ambao wana majeraha, hasa mshambuliaji hatari Amr Zaki ambaye anauguza nyonga, wakati Hossam Arafat na Sayed Mosaad hawataweza kucheza mechi hiyo. Kuna mashaka na hali ya Alaa Ali ambaye anaughua mafua.
Upinzani baina ya timu hizo mbili umekuwa wa muda mrefu kiasi kwamba umehamia hadi nje ya uwanja, ukisababisha vifo, uvunjaji wa nyumba na wakati fulani ligi nzima kufutwa.
Vurugu za mashabiki zilisababisha serikali ya Misri kupiga marufuku mechi baina ya klabu kutoka jiji moja kutumia uwanja wa klabu moja na hivyo mechi za wababe hao wawili sasa zinachezwa kwenye uwanja mmoja tu wa Cairo International Stadium.
Upinzani wao umefikia kiwango kwamba hata waamuzi wa Misri hawaaminiki na Chama cha Soka cha Misri sasa kinalazimika kutumia marefa kutoka barani Ulaya ili kuondoa upendeleo.
Mwamuzi mkongwe Kenny Clark, ambaye aliwahi kuchezesha mechi nne za Old Firm, yaani baina ya vigogo wa Glasgow nchini Scotland, Celtic na Rangers, aliteuliwa kuchezesha mechi ya watani hao mwaka 2001 baada ya vyama sita vya soka barani Ulaya kukataa kutuma waamuzi wake.
Kabla ya hapo, mechi iliyochezeshwa na mwamuzi wa Ufaransa Mark Batta, ilivunjika baada ya wachezaji wa Zamalek kugoma kuendelea na mchezo wakipinga mchezaji wao, Ayman Abdel Aziz kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika yab pili kwa kukwatua kwa nyuma.
Asili ya upinzani baina ya timu hizo unasemekana kuanzia nyakati ambazo majeshi ya Uingereza yalikuwa kwenye mitaa ya jiji la Cairo. Wakati huo, mpira wa miguu ulikuwa ukichukuliwa kama utamaduni pekee uliojipenyeza kwenye nchi ya Misri, lakini iliichukua nchi hiyo miaka kadhaa hadi 1907 ilipoanzisha klabu ya kwanza ya soka, Al Ahly, iliyokuwa ikiendeshwa na wenyeji.
Ikapewa jina la Al Ahly kumaanisha Taifa na rangi zake zikawa nyekundu ya zamani ambayo ilikuwa ikitumika kabla ya wakoloni wa Kiingereza kuvamia nchi hiyo. Al Ahly ikawa ikichukuliwa kama klabu kwa ajili ya taifa hilo, ikikutanisha watu wa kada mbalimbali na matabaka mbalimbali.
Zamalek, ambayo huvalia rangi nyeupe, ilikuwa ikichukuliwa kama klkabu ya nje na ya watui wa nje. Pia ilikuwa klabu ya mfalme ambaye alikuwa akichukiwa, King Farouk. Awali klabu hiyo ilipewa jina la mfalme huyo, lakini ikabadilishwa na kuitwa Zamalek baada ya mfalme huyo kuondolewa.
Mwanzoni timu hiyo ilikuwa na mashabiki ambao ni Waingereza na watu wa nje ambao hawakupenda mwenendo mpya wa utaifa wa Misri. Kwa hiyo upande mmoja ukawa wa rangi nyekundu yab watu maskini na wanaojivunia utaifa wao wakati upande mwingine ukawa wa matajiri, wa daraja la kati na wanaotaka mabadiliko.
Makundi hayo yapo hadi leo.
Klabu hizo mbili si bora nchini Misri tu, bali Afrika nzima huku Al Ahly ikiwa imetangazwa kuwa klabu bora ya karne na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?