Friday, November 27, 2009

 

Sita wateuliwa kusimamia uchaguzi Yanga

Sosthenes Nyoni

UONGOZI wa klabu ya Yanga umetangaza majina ya wajumbe watano watakaounda kamati itakayosimamia uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Januari 3 mwakani.

Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alisema kuwa kamati hiyo itafanya kazin kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF).

Madega aliwataja watu wanaunda kamati hiyo kuwa ni pamoja na Jaji John Mkwawa ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Ridhiwan Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Angetile Osiah , Philemon Ntahilaja na mwenyekiti wa zamani wa matawi ya Yanga asili, Yusuph Mzimba.

Alisema kuwa uteuzi huo umezingatia katiba ya klabu hiyo iliyofanyiwa marekebisho Agosti 8 2006 iliyotaka kamati ya uchaguzi kuwa na watu wasiopungua watano na wasiozidi saba.

"Uteuzi wa majina haya umezingatia katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho Agosti 8 2006 ambapo inaelekeza kuwa kamati ya uchaguzi inatakiwa kuwa na watu wasiopungua watano na wasiozidi saba,"alisema Madega.

Aliongeza kuwa uongozi wa klabu hiyo utakutana na wajumbe hao ili kuelezana majukumu yanayotakiwa kufanywa wakati wa zoezi hiyo la uchaguzi.

Madega, pia aliwataka wanachama wa klabu hiyo kutumia haki yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa kuhakikisha wanalipa ada za uanachama wao ili wawe wanachama hai na wenye sifa za kushiriki uchaguzi.

"Haki mojawapo ya mwanachama ni kuchagua kiongozi anayemtaka, hivyo natoa wito kwa wanachama ambao hawajamaliza ada za uanachama wao walipe ili wawe na sifa ya kushiriki katika uchaguzi,"alisema Madega.

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?