Tuesday, November 13, 2007
Eti Kamati ya Bayser inaadhibu kama Fifa/Caf?
Eti kamati ya Bayser inaadhibu kama Fifa, CAF!
Na Angetile Osiah
ZINEDINE Zidane na Marco Materrazi waliitwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kwenda kujibu shtaka lao lililotokana na sakata lililotokea katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia.
Roy Keane aliitwa na Chama cha Soka cha England (FA) kujibu tuhuma za kutaka kuvuruga mchezo wa soka wakati alipoandika kitabu chake cha maisha ya soka, akiwa ameeleza kwenye kitabu hicho kuwa alimchezea rafu kwa makusudi mchezaji wa timu pinzani.
Na Dean Saunders, mshambuliaji wa zamani wa Liverpool na Aston Villa, alifungua kesi mahakamani akitaka alipwe fidia baada ya kuchezewa rafu ya makusudi iliyokatisha soka lake alilokuwa akilitegemea kwa maisha yake.
Na wachezaji sita wa Arsenal na wawili wa Manchester waliitwa kujieleza mbekle ya FA kutokana na vurugu zilizotokea katika mechi yao ya Ligi Kuu na waliadhibiwa kwa kufungiwa kucheza mechi na kupigwa faini sambamba na klabu zao.
Hayo ni mazingira tofauti yanayotokea kwenye soka na ambayo yanafanyiwa uamuzi tofauti kutoka katika vyombo tofauti. Hiyo ni kujaribu kuelezea kuwa sheria za soka zinatakiwa kuendana na hali na mazingira ya sehemu zinapotumika na si eti kufuata kile Fifa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) linachoamua.
Msingi wa hoja zangu za leo ni adhabu mfululizo ambazo zimekuwa zikitolewa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka (TFF) dhidi ya wachezaji, waamuzi na viongozi bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea.
Haruna Moshi alifungiwa mechi sita, Athuman Iddi miezi mitatu, Bernard Mwalala mechi sita, na wengine wengi, wakiwemo waamuzi ambao wameondolewa kabisa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu.
Ni kweli kwamba TFF imepania kupambana na vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikichangia sana kutoendelea kwa soka letu. Lakini inaonekana kuwa mkakati huo unatafsiriwa vibaya na watendaji, na hasa Kamati ya Mashindano, ambayo imetumia mwanya huo kuwabandika virungu wachezaji, viongozi na waamuzi bila ya kuwasikiliza.
Wiki hii tulijaribu kupata ufafanuzi kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Jamal Bayser, ambaye alijibu kifupi tu hawawezi kuwaita watuhumiwa kwa sababu wanachofuata ni taarifa ya refa na kamisaa tu.
Ni kweli kuwa mwamuzi wa mwisho katika soka ni refa, lakini inapotokea matatizo ambayo ni nje ya sheria zake, basi ni lazima wahusika waitwe kutoa ushahidi.
Kwa mfano, kamati haiwezi kubatilisha uamuzi wa kumuonyesha kadi nyekundu mchezaji kwa kuwa hilo hutokea ndani ya dakika tisini, ingawa kwa wenzetu hilo sasa linawezekana baada ya kamati ya nidhamu kuangalia upya mkanda wa video na inapobaini kadi haikuwa halali inaifuta.
Lakini kwa kuwa teknolojia yetu bado iko chini, tutaendelea kuheshimu maamuzi ya refa kama ambavyo Fifa na CAF inaheshimu kutokana na kusita kuanza kutumia teknolojia zaidi ili ubinadamu uendelee kuwepo kwenye soka, yaani makosa ya mwamuzi ni sehemu ya ubinadamu ambao unatakiwa kuheshimiwa mchezoni.
Lakini inapotokea katika taarifa yake, refa anasema alitishiwa na mchezaji, basi madai yake ni lazima yafanyiwe kazi ili ukweli uonekane uko wapi. Ronaldo alishtakiwa kwa kumtukana refa, lakini alipoitwa alikiri kutumia maneno ambayo kwa Kireno ni matusi, lakini akajieleza kuwa hutumia maneno hayo kujijutia na hivyo adhabu yake ikawa ndogo.
Kama asingeitwa, FA isingefikiria kumpa adhabu kama hiyo. Leo hii, Roy Keane ameshtakiwa kwa kosa la kuwaghasi waamuzi wakati wa mechi, lakini na yeye ameripoti FA kuwa mwamuzi aliyechezesha pambano hilo alimtukana. Bila ya Keane kupata nafasi hiyo ya kujieleza, ingefahamika vipi kuwa kumbe alitukanwa.
Hatuwezi kung'ang'ania kuwa refa ni mtu safi anayeweza kusema ukweli bila ya kuweka chumvi kwa nia ya kujilinda au kunufaisha upande mmoja.
Kama kibendera alikataa bao ambalo lilifungwa kutokana na mpira wa kurusha na refa akalikubali eti kwa sababu mchezaji aliotea, lazima mfungaji atajikuta akipanda hasira haraka kwa kuuliza ni refa gani anayeweza kukubali goli la aina hiyo. Ndiyo yaliyomkuta Mwalala.
Unapomuadhibu refa huyo kwa kufanya uamuzi huo wa ajabu, unamuweka wapi mchezaji aliyefanya kosa kutokana na kupandishwa hasira na tukio hilo. Mwite ajieleze ndipo ufikirie adhabu ambayo anastahili kulingana na jinsi alivyochokozwa hadi akatenda kosa na ndio maana kuna makosa ya mauaji na mauaji ya kukusudia ambayo adhabu zake hutofautiana kulingana na mazingira.
Kimsingi, kama Bayser anasema hivyo, maana yake hata hiyo kamati yake kukutana haina maana kwa kuwa tayari adhabu zipo kulingana na kosa lililosemwa na refa. Kinachotakiwa hapo ni kutangaza tu adhabu bila ya kuitisha kikao.
Nachotaka kueleza hapa ni kwamba Tanzania ni nchi ambayo ina utamaduni wake na ina njia zake za kupambana na matatizo yanayokwamisha maendeleo ya soka, na Fifa na CAF zinatoa tu mwongozo wa jinsi ya kushughulikia matatizo hayo bila ya kwenda nje ya kanuni na sheria zake.
Kwa hiyo, TFF na hasa hiyo kamati ya Bayser, haina budi kuandaa taratibu na kanuni za kuadhibu wachezaji kwa kutumia mazingira yetu. Adhabu zinazotolewa sasa hazitaweza kusaidia kukomesha utovu wa nidhamu kama walengwa wataona waliadhibiwa bila ya kutumia haki au waliadhibiwa bila ya masuala yao kuzingatiwa, yaani jinsi kosa lilivyotokea.
Adhabu zitakuwa na maana tu kama wahusika watashiriki katika sehemu fulani ya mchakato wa kutoa uamuzi na hapo ndipo wataweza kujua kuwa masuala yao yalizingatiwa kwa kiasi fulani hata kama wanajua kuwa ni kweli walifanya makosa.
Kutumia mfumo wa Fifa na CAF ni kujidanganya kwa sababu si rahisi kwa vyombo hivyo viwili kumuita mchezaji kama Athuman Iddi aende kujitetea Fifa au CAF kwa kosa alilolifanya nje ya uwanja wakati wa mechi za vyombo hivyo kwa kuwa itakuwa ni vurugu.
Lakini chama cha nchi ni lazima kifanye hivyo kwa kuwa gharama zinakuwa ndogo kulinganisha na zile za kwenda Cairo au Zurich ambako vyombo hivyo vinashughulikia si matatizo ya nchi au mchezaji mmoja, bali karibu nchi 200 kote duniani.
Kwa hiyo, Bayser na kamati yake wasijaribu kukwepa masuala ya msingi kwa kusingizia eti kufuata mfumo wa Fifa na CAF. Waangalia mazingira ya nchi yetu na nini hasa kinahitajika katika kufanikisha mkakati wa TFF wa kupambana na utovu wa nidhamu.
Angetile Osiah
0754 887 222