Monday, October 15, 2007

 

Wanaopinga, wajibu hoja za Madega

Na Angetile Osiah
KUNA kila dalili kuwa wakati wa kutotumia busara kuamua mambo umewadia kwa wanachama wa klabu kongwe ya Yanga kama ilivyokuwa mwaka 1994 wakati suala la kampuni lilipoibuka baada ya wafadhili watano kuachia ngazi katika jitihada za kushinikiza katibu wa wakati huo, George Mpondela aachie ngazi.

Ilikuwa ni kipindi kigumu kwa uongozi wa Mpondela, ambaye wakati huo alionyesha msimamo mkali uliofanya apachikwe jina la 'Castro' kutokana na kutokubali kunyenyekea wafadhili hao na kuwaruhusu wawakalie viongozi mabegani.

Wale waliopingana naye hawakutaka kutumia akili na busara zao, na badala yake waling'ang'ania sentensi moja tu kuwa "mpira wa sasa bila ya fedha, hauwezekani" hivyo lazima Mpondela na kundi lake wasalimu amri.

Lakini Mpondela aliungwa mkono na wengi waliojitokeza kupinga vitendo vya wafadhili hao, wajkiongozwa na Marehemu Abbas Gulamali, kumuwekea vikwazo ili ashindwe kuiongoza Yanga na umuhimu wao uonekane ili warejeshwe.

Ilifikia wakati wanachama hao walioweka kando busara zao walidiriki kumbeba Gulamali kumrejesha klabuni kwa nguvu, lakini kundi lililomuunga mkono Mpondela lilikuwa kubwa zaidi na hivyo kufanikiwa kuendelea kushika klabu.

Hujuma, ambazo kwa kawaida huwa hazijipenyezi kwenye timu kila inapotokea mgogoro kwenye klabu ya Yanga, ziliingia kwa kiasi fulani na Yanga ikapoteza mechi moja kabla ya timu kutekwa na wafadhili hao, lakini iliporejea uwanjani ikiwa imehudumiwa kila kitu na wafadhili, ilikung'utwa mabao 3-0 na Sigara kwenye Uwanja wa Taifa.

Ilidhihirika kuwa kuwepo kwa wafadhili hakumaanishi matokeo mazuri uwanjani na timu ikarejeshwa kwa Mpondela na ni wakati wa sakata hilo, Yanga ikawa tishio na kama si 'gundu' ingeweza kufika mbali Afrika, ikiwa na majina kama Constatine Kimanda, Ngandou Ramadhan, Shaaban Nonda, Method Mogella, Steven Nyenge, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Maalim Saleh, Anwar Awadh na wengine wakongwe kwa chipukizi na timu ilikuwa ikifundishwa na Mcongo, Tambwe Leya baada ya Charles Boniface kuiongoza kwa mafanikio mwaka uliokuwa umetangulia.

Majina hayo makubwa yalikuwa yamesajiliwa na wafadhili hao, lakini wakataka kuwakalia viongozi mabegani, baadhi ya wafadhili wakitaka kuchapisha kadi za wanachama zenye picha zao, wengine wakiingilia utendaji wa shughuli za kila siku, wengine wakidiriki hata kusema kuwa timu ililazimisha sare Dodoma baada ya refa kupewa fedha ili aongeze muda, kitu kilichomaanisha dharau kwa kocha na wachezaji.

Vituko vilikuwa vingi, kiasi kwamba kundi lililokerwa na ufadhili hilo lilijitokeza na kumuunga mkono Mpondela.
Hali haionyeshi kuwa na mabadiliko sana. Wakati ule wafadhili ndio waliokuwa wakipinga wazo la kampuni na kuwapa fedha wale waliopiga kelele kuwa Yanga ijitegemee. Lakini safari hii ni tofauti ya kimtazamo tu.

Hakuna Yanga Asili wala Kampuni, lakini tofauti iliyopo ni ile ya jinsi ya kutekeleza wazo hilo.Vinara wa makundi hayo wamebadilika, lakini wale wanaosukuma kuwepo kwa hali hiyo ni wale wale waliokuwepo wakati wa mgogoro wa mwaka 1994. Angalia televisheni au soma magazeti utaona walio katikati ya mgogoro huo ni wale wale waliosumbua mwaka 1994.


Hali ya kufanana pia ipo kwenye timu, yaani idadi kubwa ya wachezaji imesajiliwa na mfadhili, na kama ilivyokuwa kwa akina Ndonda, Ngandou, Kimanda na Method, ambaye alinunuliwa toka Simba, safari hii wapo Laurent Kabanda, Bernard Mwalala, Maurice Sunguti, Aime Lukunku na Athuman Iddi, ambaye alichukuliwa Simba.

Kama nilivyosema tofauti ni mtazamo au njia ya utekelezwaji wa jinsi ya kuhamisha timu kutoka kwenye uongozi wa klabu kwenda kwenye uongozi wa kampuni, ambao nahisi haupo.

Mwenyekiti Imani Madega alijitokeza mapema wiki hii na kueleza jinsi alivyotofautiana kimtazamo na mfadhili, ambaye pia ni mdhamini wa Yanga, Yusuf Manji, katika zoezi zima la utekelezwaji wa suala hilo. Ameeleza jinsi klabu inavyokosa uwakilishi wa kutosha kwenye kampuni licha ya kuwepo kwa maneno kuwa ndiyon itakayomiliki asilimia 51 za hisa.

Ameeleza udhaifu wa katiba na jinsi walivyowasiliana na Manji kuhusu kuzirekebisha kasoro hizo kwa njia ya kuunda kamati ndogo ili marekebisho hayo yafanyike katika muda usiopungua miezi mitatu, na ameeleza jinsi klabu itakavyokuwa na hisa saba tu zenye thamani ya Sh 7,000.

Pia amechambua udhaifu wa rasimu ya muafaka, ambayo imejumuishwa kwenye katiba mpya na kuwa sehemu ya katiba na jinsi alivyowasiliana na Manji juu ya njia za kuondoa udhaifu huo na haja ya kuwepo uwazi katika suala zima la utekelezwaji wa mpango huo.

Pia ameeleza jinsi ilivyokuwa tatizo kutekeleza zoezi la kusajili wanachama katika muda wa siku nane tangu Manji atoe barua ya kukubali kutoa Sh milioni 10 alizoombwa kwa ajili ya zoezi hilo, akisema kuwa uongozi ulitaka kuangalia jinsi ya kulifanya zoezi hilo ili fedha zitakazotolewa na wanachama kulipia ada ziingie kwenye mifuko sahihi ya klabu.

Hata sharti la kukabidhi timu siku moja tu baada ya uchaguzi, nalo lilikuwa na mashaka, kama alivyoeleza Madega.
Na la mwisho ambalo hakulisema lakini ambalo linazungumzwa ni jinsi Manji anavyoshupalia suala la timu kuhamishiwa kwenye kampuni bila ya kulishupalia kundi la kampuni kukamilisha taratibu za usajili wa kampuni ili iweze kuwa tayari kukabidhiwa timu.

Ni kweli kuwa kampuni bado haijakamilisha usajili tangu ilipokubaliwa kuwa muundo wa kampuni ubadilike tofauti na ile iliyosajiliwa awali wakati Manji hajaingia kusuluhisha makundi yaliyokuwa yanapingana.

Nilidhani kuwa hoja hizo za Madega zingezua mjadala na wale wanaompinga wangefanya jitihada za kuzijibu ili waonyeshe kuwa amekosea, lakini badala yake nilishangazwa kuona taarifa ya viongozi wenzake ikimkana Madega bila ya kujibu hata hoja moja alizozitoa.
Taarifa hiyo ya juzi inaonyesha kumnyenyekea zaidi Manji na kukwepa kabisa kuzungumzia kasoro ambazo Madega alizionyesha katika kutekeleza utashi wa Manji wa kutaka timu ikabidhiwe kwa kampuni na klabu kuongeza wanachama ili ijenge mtaji wake.
Kutozungumzia hoja za Madega ni kuipumzisha akili kufanya mambo ambayo yangeisaidia klabu. Binafsi naona hoja za Madega zina nguvu na wakati huu wanachama wanapoibuka kumuomba msamaha Manji kwa kauli za Madega na kumshutumu mwenyekiti wao, wangeonyesha ni kwa vipi hoja za Madega si za msingi na zoezi la kuikabidhi timu litatekelezwaji bila ya kuzingatia hoja hizo.
Ni kweli Yanga inamuhitaji Manji kama inavyohitaji wadhamini wengine, lakini inapoonekana kuna matatizo ni vizuri yachunguzwe na kuwekwa sawa ili mambo yaende bila ya matatizo.
Tujibu hoja za Madega na si kurushiana matusi na kuviziana.

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?