Thursday, April 27, 2006

 

Waziri Bendera, mengi yanakusubiri michezoni

KWA mapitio ya haraka haraka tu ni kwamba karibu kila mpenda michezo amefurahishwa na uteuzi wa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, Joel Bendera kuwa naibu waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, ambaye anajikita zaidi kwenye michezo.
Naweza kuhisi kuwa kukubalika kwa uteuzi huo kunatokana na ukweli kwamba Bendera, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kabla ya kuvuliwa siku moja kabla ya uchaguzi mkuu Desemba 14 kutokana na kumaliza muda wake, ni mwanamichezo halisi ambaye ameshiriki kwa kiasi kikubwa kujaribu kuinua michezo na hasa soka.
Kwa maana hiyo, kupewa dhamana ya kuongoza michezo ni uteuzi mwafaka na ambao umekuja kwa wakati muafaka.
Kwanza ana shahada ya pili ya elimu ya viungo, akiwa amejikita zaidi katika ualimu wa soka, ana diploma ya ualimu wa soka, amepitia kozi mbalimbali za uongozi wa michezo na ameshakuwa mwalimu wa soka, na cha zaidi ameshakuwa mwaliku wa Chuo cha Elimu Korogwe.
Hayo peke yake yanaonyesha ni kiasi gani, wizara hiyo imempata mwenyewe.
Lakini Bendera, ambaye atakuwa chini ya Waziri Mohamed Seif Khatib, anaingia madarakani wakati kukiwa na mabadiliko mengi na hasa kwenye katiba za vyama vya michezo na klabu zikiwa zimefanyiwa marekebisho makubwa.
Tena mabadiliko hayo ni yale yanayoiondoa serikali katika shughuli za vyama hivyo na klabu, na kama Mheshimiwa Bendera atakumbuka mgogoro wa mwisho aliopambana nao ni huu wa Chama cha Riadha Tanzania (TAAA), ambacho sasa kimejibadilisha jina na kuwa AT.
Kuondolewa kwa serikali kwenye katiba za vyama hivyo kunalifanya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuonekana linaondokewa na majukumu ambayo iliyazoea.
Sasa BMT haina mamlaka yoyote juu ya vyama vingi vya michezo, likiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Kikapu (TBF), lakini sheria ya nchi bado linaitambua BMT kama chombo cha serikali chenye maamuzi ya juu katika michezo kabla ya waziri husika.
Ni kwa maana hiyo ndiyo nafikiri kuwa Mheshimiwa Bendera atakuwa na kazi ngumu ya kutafsiri upya majukumu ya BMT katika usimamiaji michezo baada ya mabadiliko hayo ya vyama na hasa katika kipindi hiki, ambacho Mheshimiwa Rais, Jakaya Kikwete ameahidi kusaidia vyama katika sekta ya ufundi.
BMT itakuwa na nafasi gani ya kuhakikisha msaada huo wa serikali unatumika ipasavyo kama vyama havilitambui tena baraza hilo.
Lakini Bendera pia ameingia wakati ambapo serikali imeahidi kurudisha michezo mashuleni. Hapa Bendera na waziri wake watakuwa na kazi ngumu ya kutengeneza tena mkakati wa kuhakikisha michezo inafundishwa vipi mashuleni kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu.
Tunajua pia kuwa serikali haitakiwi kulazimisha michezo kuendeshwa kwa malipo (professional) bali vyama husika kama soka, ngumi na kikapu, lakini inaweza kujenga mazingira yatakayowezesha michezo kuwa ajira ya uhakika.
Na hili litawezekana kama Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo itakaa pamoja na wenzao wa Wizara ya Kazi kufikiria kuweka mazingira ambayo yataifanya hiyo ajira, ambayo inasemekana imeshajengwa kwenye michezo kama soka na ngumi, kuwa ya uhakika.
Kuandikiana mikataba ya kulipana fedha kana kwamba za kusaidia, hakufanyi soka kuwa ya kulipwa. Ukweli kwamba wanasoka wanategemea mchezo huo kuendesha maisha yao hakufanyi soka ikawa ya kulipwa.
Kuna mambo muhimu ambayo yanatakiwa yaangaliwe na wizara hizo mbili na pengine hata ile ya fedha kuhakikisha kuwa soka na michezo mingine yenye uwezo wa kuvuta mashabiki wengi, wadhamini na kuingiza fedha, inatengeneza ajira zenye uhakika na za kudumu.
Pia vyama kwa sasa vina mikakati yake ya muda mrefu ya maendeleo, ambayo kwa kiasi fulani yatakuwa na manufaa kwa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa maana hiyo serikali lazima iweke mkono wake kuhakikisha malengo hayo yanafanyika.
Huu ni wakati wa kuangalia serikali itajihusishaje licha ya kwamba vyama hivyo vimeiondoa serikali katika shughuli zake.
Yapo mengi sana ambayo Mheshimiwa Bendera na bosi wako mtatakiwa myaangalie kwa makini wakati mtakaposhika ofisi zenu kuanzia Jumatatu.
Sisi wapenzi wa michezo tumekaa kusubiri kuona kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya inatafsiriwa vipi katika utendaji.

Comments:
Karibu mtandaoni mzee wa Ujerumani tuna uhakika kwamba tutafaidika na fikra makini za kiuana michezo, lakini pia za kijamii na kisiasa.

Michezo limekuwa eneo moja lenye utata na matatizo makubwa katika ustawi wake nchini hivyo tuna imani mabadilishano ya mawazo kati yetu wana blogu yatasaidia katika kusukuma mbele ustawi wake na hivyo kusongesha mbele taifa.

Kwani Jamaica au Brazili wana nini cha maana kama siyo michezo. Kwanini na sisi tusiwe kama wao?
 
Angetile ngubwene. Segelela nkamu gwangu.

Ujio wako ni mapinduzi makuu hasa nikizingatia umakini wako katika fani uliyobobea kwayo - michezo na burudani.

Alan wasalaan sana.
 
Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?