Friday, April 28, 2006

 

Nani aingie kudhamini klabu zisizo na uhakika

MIAKA minne iliyopita nilitumwa Arusha kwenda kuandika habari ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Arusha FC.
Kama kawaida niliondoka asubuhi Dar es Salaam na kufika Arusha majira ya saa 11.00 jioni na kwa kuwa lazima wageni wapewe nafasi ya kutumia uwanja siku moja kabla ya mechi, nilipitiliza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuangalia mazoezi ya Yanga.
Lakini cha kushangaza nilikuta vijana wa Rolling Stones wakiendelea na mazoezi.
Nilikuwa mmoja wa umati wa watu walioshikwa na butwaa kutoiona Yanga na ambao moja kwa moja waliingiwa na wasiwasi kuwa mechi hiyo ambayo ingefanyika Jumamosi, yaani kesho yake.
Nilipomuuliza mmoja wa viongozi wa soka wa Arusha kuhusu kutofika kwa Yanga, yeye ndiye aliyenishangaa kwamba eti sina taarifa kuwa mechi hiyo imearishwa hadi wikiendi iliyokuwa inafuata.
Gharama ambazo kampuni yangu ya wakati huo iliingia kwa ajili ya kupata taaifa za mechi hiyo, zilikuwa zimekwenda bure na nililazimika kuanza kuandaa safari ya kurudi Dar kuendelea na shughuli nyingine.
Hayo ndiyo matatizo yanayokumba wadau wengi wa soka - mambo kuendeshwa bila ya kutabirika na hivyo kutokuwepo kwa mipango itakayowezesha wadau kuhusika kwa njia moja au nyingine katika mechi za soka.
Mechi ya soka haihusu timu mbili zinazokutana peke yake, bali wadau wengine wote wanaozunguka mchezo huo - yaani wafanyabiashara wadogo kwa wakubwa, vyombo vya habari, wadhamini na watu wengine wote wanaoweza kutumia soka kuendesha maisha (lakini si kwa ujanja ujanja).
Kwamba unapokuwa umepanga mechi itafanyika Desemba 20 mwaka huu na usiibadili tarehe, maana yake vyombo vya habari vitaweza kujipanga jinsi ya kuishughulikia mechi hiyo - kwa njia moja kupata wateja wengi zaidi na kwa njia nyingine kuhamasisha umma.
TV zitaweza kufikiria kama zitaweza kununua haki za kutangaza mechi hiyo, wakati bendi zitafikiria jinsi ya kujinufaisha kwa kwenda kufanya onyesho mkoani humo jioni ya siku ya mechi. mahoteli yatafikiria jinsi ya kupata wateja watakaoenda kuangalia mechi hiyo na wadhamini watafikiria jinsi ya kudhamini timu hizo ili wajitangaze kibiashara.
Kuna mambo mengi yanayoonyesha kuwa mechi moja ya soka inahusu mambo mengi kwa maana hiyo kuwa na uhakika wa kueleweka kuwa mechi itafanyika siku fulani kunatoa mwanya kwa wadau kujipanga vizuri.
Leo hii ushiriki wa Yanga na Simba kwenye michuano ya Kombe la Kagame hauko bayana, hivi nani anaweza kuanza kujipanga kibiashara, kikazi au kijamii kwa ajili ya mashindano hayo?
Hivi mdhamini gani ataweza kuingia na kuweka fedha zake kuidhamini Yanga au Simba kwenye michuano hiyo wakati hadi sasa klabu hizo bado zinatoa kauli zisizoeleweka kuhusu ushiriki wao kwenye Kagame?
Kama Yanga hadi jana imesema haitashiriki michuano hiyo, itawezaje kupata wadhamini katika hali kama hiyo.
Klabu zetu lazima zijifunze kuwa wakati ule wa kujiendesha kiholela umekwisha.
Viongozi wa klabu hizo hivi sasa walitakiwa wawe wanazunguka kwenye makampuni kujaribu kuyashiwishi jinsi yatakavyonufaika na mashindano ya Kagame iwapo yatadhamini klabu hizo kutokana na ushindani ulio katika mashindano hayo na jinsi zilivyo na mvuto.
Hiyo asilimia 25 ya mapato ambayo klabu hizo zinadai zitakuwa kubwa kiasi gani kama hata mashabiki hawana uhakika wa ushiriki wa timu hizo katika michuano ya Kombe la Kagame?
Kwa karibu misimu mitatu sasa, Yanga inashiriki Ligi Kuu bila ya mdhamini wa kueleweka na hii itaweza kuendelea kama uongozi hautakuwa imara katika mambo yake na kuwa unatoa kauli zinazochanganya hata hao wanaofikiria kuidhamini.
Klabu hizi mbili hazina budi kuanza sasa kuwa na mipango ya muda mrefu na iliyo imara ili ziweze kushawishi wadhamini kutumbukiza fedha zao kwenye klabu hizo, lakini pia kuwafanya mashabiki waweze kujipanga vizuri kwa ajili ya mechi zao ili zinufaike kwa mapato.
Wasipobadilika wataendelea kugombea mapato ya milangoni, ambayo kwa klabu kubwa ni sehemu ndogo sana ya mapato ya kuendeshea klabu.

Comments:
Welikamu! welikamu! msisitizo kwa kimombo.
Jurunzi karibu katika ulmwengu huu wa blogu.Mambo kibao toka kwako tunayategemea
 
Karibu sana. Sasa kijiji kinapanuka zaidi kwa kuwa na wanavijiji waliobobea kwenye masuala ya michezo. Najua katika mambo ambayo taifa letu linahitaji kutazama kwa undani ni michezo. Tunatakiwa tujiulize kwanini tuwe na taifa ambalo watoto wake wanacheza mpira wa makaratasi barabarani au mashambani? (kama nilivyokuwa nafanya kule Moshi).

Karibu ndugu yetu.
 
Oya mzee karibu, nikipanda kwangu baadaye nitakurusha huko ili umma na wasomaji wa Gazeti Tando langu wakusome na kuja kukusalimia hapa.
 
Angetile ngubwene. Segelela nkamu gwangu.

Ujio wako ni mapinduzi makuu hasa nikizingatia umakini wako katika fani uliyobobea kwayo - michezo na burudani.

Kama alivyosema Ndesanjo na Mzee wa Mshitu, kwa nini fani ya michezo na Burudani inapewa kipa-unyuma. Yaani tunachezea makaratasi halafu tunatarajia kushindana na wakina Beckham na Ziddane siku za mbele. Jamaica inajulikana kwa muziki wa Reggae Brazil inajulikana kwa soka. Tanzania itajulikana kwa lipi ikiwa hata taaluma tumezidiwa hata na Kenya. Michezo na Burudani vyaweza chukua nafasi sasa.

Alan wasalaan sana.
 
Karibu sana.Usijisikie uko nyumbani maana ukifanya hivyo unaweza ukaamua kulala..jisikie uko kazini ili tuendeleze mapinduzi haya.
 
Sikuingia hapa kuchanguia hoja hii, kwa leo naingia kukukaribisha Mr Ngeta. Karibu sana. Napoanza mchezo huu wa kublogu, hutaacha katu, 'nisawa na kula nyama ya mtu'-JK Nyerere)
 
Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?